Nyumbani > Katiba > Tamko la Mtandao wa Wanawake na Katiba
Prof.Meena2

Sisi, Mtandao wa Wanawake na Katiba pamoja na asasi zisizo za kiserikali zipatazo 50 na watu binafsi tunaoshughulikia masuala ya kijamii kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanazibar, tumekutana Royal Village Hotel, Dodoma mnamo tarehe 31 Augusti hadi 1Septemba kujadili haki za wanawake katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huu ni muendelezo wa harakati za kuhakikisha kwamba wanawake wanatoa sauti ya pamoja ya kudai Katiba mpya inyozingatia mrengo wa kijinsia.

Sisi wanawake tunatambua kuwa Katiba inayozingatia mrengo wa kijinsia ni ile iliyotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake na wanaume, na iliyoweka bayana makubaliano na msingi mkuu unaoongoza nchi yetu. Vilevile ni Katiba iliyojengewa msingi wa usawa, utu na heshima ya mwanamke na mwanaume na inayokataza aina zote za ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia.

Sisi, wanawake wa mtandao huu tunasisitiza kuwa mchakato wa kuleta Katiba mpya ufanyike kwa kutambua kuwepo kwa:

• Ubaguzi wa kijinsia unaoathiri upatikanaji wa haki za msingi za wanawake uliyojikita katika misingi ya ubaguzi wa jinsia.
• Ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu na hususani wanawake wenye ulemavu
• Ukiukwaji wa haki za watoto na ubaguzi wa watoto wa kike,

Kwa kuzingatia haya, mtandao wa wanawake na Katiba bado tunaendelea kusisitiza madai muhimu ya wanawake kama yafuatayo:

• Katiba mpya ikiri kuwa moja ya tunu za taifa ni usawa wa kijinsia.

ARDHI NA RASLIMALI
• Katiba mpya iwe na kipengele kinachoainisha kuwa mwanamke ana haki sawa ya kumiliki, kupata, kutunza, kutumia, kuhamisha na kurithi ardhi na rasilimali za taifa.
• Katiba mpya iweke misingi ya kutambua kumiliki rasilimali na ardhi kwa wanawake wenye ulemavu
• Kuwepo na chombo huru kitakachokuwa na ilani ya kusimamia haki ya mwanamke katika kumilika na kufikia rasilimali kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa
• Katiba ihakikishe kuwa Mikataba ya uwekezaji katika ardhi na rasilimali iwe shirikishi kwa wanawake na wanaume, iwe ya muda mfupi yenye lugha ya Kiswahili na vipengele vinavyomnufaisha mwanamke kiuchumi

UMRI WA MTOTO
• Katiba itamke wazi umri wa mtoto ni kuanzia kuzaliwa hadi miaka 18 na kutokuwepo kwa ndoa chini ya miaka hiyo
• Katiba mpya iweke misingi ya kulinda watoto wenye ulemavu kulindwa mpaka pale watakapo kuwa na uwezo wa kushiriki ipasavyo kwenye mambo ya kijamii
• Katiba itambue Utu wa mtoto wa kike
• Katiba ihakikishe kuwa Sheria zinazomhusu mtoto wa kike hazikinzani

HAKI ZA HUDUMA MUHIMU
• Katiba mpya iweke haki ya elimu bora na bure kufikia darasa la kumi na mbili (12)
• Katiba ihakikisha kunakuwepo kwa Haki ya kupata huduma bora, bure na salama ya uzazi na isiyo na vikwazo
• Katiba ihakikshe kuwa kunapatikana kwa Haki ya huduma bora , salama, na ya wakati kwa wanawake na wanaume
• Katiba mpya itamke kuweka mikakati maalum ya kuwezesha wanawake wenye ulemavu kupata haki na kunufaika na huduma za kijamii
• Katiba mpya itamke utekelezaji wa sheria na mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu haki za wanawake na walemavu iliyoridhia
• Katiba inahakikisha kuwepo kwa Haki ya msingi ya kupata maji safi na salama kwa kila kaya na kwa gharama nafuu

UONGOZI 50/50
• Katiba mpya izingatie 50/50 kwa ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi ya kijiji mpaka taifa kwenye serikali kuu
• Katiba mpya iunde chombo au tume itakayoweza kusimamia na kuhakikisha usawa wa kijinsia unatekelezeka katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii
• Katiba mpya iweke misingi ya 50/50 kwenye ngazi za maamuzi ikizingatia uwakilishi wanawake na walemavu.
• Katiba iunde Tume itakayosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Imetolewa 1 Septemba 2014
Dodoma

Maoni, RSS

  • Mrembo

    says on:
    12/09/2014 at 5:47 pm

    Wanawake mmefanya kitu cha msingi sana.. Mbarikiwe

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*